AZIZ KI APIGA HAT TRICK YANGA YAICHAPA KAGERA SUGAR 5-0


MABINGWA watetezi, Yanga SC wamepiga hatua kubwa katika kampeni ya kutwaa tena taji hilo baada ya kuitandika Kagera Sugar mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Nyota ya mchezo wa leo ilikuwa upande wa kiungo wa Kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki aliyefunga mabao matatu pele yake, huku mengine yalifungwa na mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele na winga Mghana, Bernard Morrison.
Aziz Ki alifunga bao la kwanza kwa penalti dakika ya 42 baada ya Mayele kuangushwa kwenye boksi, la pili kwa shuti la umbali wa mita 30 na dakika ya 45 na ushei la tatu kwa penalti pia kufuatia Clement Mzize kuangushwa kwenye boksi pia dakika ya 90.
Mayele alifunga dakika ya 49 baada ya kuwatoka mabeki wa Kagera na kumchambua kipá Said Kipao na Morrison akafunga kwa shuti la umbali wa mita 18 dakika ya 84.
Yanga sasa wanafikisha pointi 68 na kuendelea kuongoza Ligi kwa pointi nane zaidi ya watani, Simba SC baada ya wote kucheza mechi 25, wakati Kagera Sugar wanabaki na pointi zao 32 za mechi 26 nafasi ya nane.
Mechi ijayo ni dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC Jumapili ijayo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post