YANGA OYEEE, YATINGA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA


TIMU ya Yanga SC ya Tanzania imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Marumo Gallants usiku huu Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng NW Jijini Rustenburg nchini Afrika Kusini.
Ilikuwa siku nzuri ofisini kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fiston Kalala Mayele aliyefunga bao la Kwanza dakika ya 45, kabla ya kumsetia Mzambia, Kennedy Musonda kufunga la pili dakika ya 62.
Marumo Gallants walipata bao lao pekee kupitia kwa mshambuliaji wao, Ranga Piniel Chivaviro dakika ya 90 na ushei, hivyo kuendelea kufungana na Mayele kwneye chati ya ufungaji kila mmoja akiwa na mabao saba.
Yanga wanakwenda Fainali kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kuwafunga Marumo Gallants 2-0 kwenye mchezo wa Kwanza Jumatano iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Yanga itakutana na mshindi wa jumla katí ya ASEC Mimosas na USM Alger zinazorudiana usiku huu Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers baada ya sare ya 0-0 kwenye mechi ya kwanza Jumatano iliyopita Uwanja wa Bouaké Jijini Bouaké nchini Ivory Coast.
Ikumbukwe Fainali za Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu zitapigwa Mei 28 na Juni 3 nyumbani na ugenini.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post