WENYEJI, Manchester United jana wamepata ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuilaza Copenhagen 1-0 Uwanja wa Old Trafford Jijini Manchester.
Bao pekee la Manchester United katika mchezo huo wa Kundi A limefungwa na beki wa Kimataifa wa England, Harry Maguire kwa kichwa dakika ya 72 akimalizia kazi nzuri ya kiungo Mdenmark, Christian Eriksen.
Ikawa siku nzuri pia kwa kipa Mcameroon, Andre Onana aliyeokoa mkwaju wa penalti wa Jordon Larsson dakika ya 90 baada ya Scott McTominay kumchezea rafu Mohamed Elyounoussi wa Copenhagen.
Ushindi wa kwanza kundini unaifanya timu hiyo ya kocha Mholanzi, Erik ten Hag ifikishe pointi tatu katika mchezo wa tatu tatu na kusogea nafasi ya tatu ikizidwa pointi moja na Galatasaray, wakati Bayern Munich yenye pointi tisa inaongoza.