KLABU ya Simba SC imetangaza kuachana na Kocha wake Mbrazil, Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo 'Robertinho' (63) baada ya miezi 10 tu kazini tangu alipowasili Januari 13, mwaka huu akitokea klabu ya Vipers ya Uganda.
Taarifa ya Simba SC mchana huu imesema kwamba pamoja na Robertinho, pia kocha wa Fiziki, Mnyarwanda Cornoille Hategekimana naye ameondolewa na kwamba hivi sasa kitakuwa chini ya Mspaniola, Daniel Cadena aliyekuwa kocha wa makipa ambaye atafanya kazi pamoja na kocha wa timu za vijana, Suleiman Matola.
Hatua hiyo inakuja siku mbili tu baada ya SImba kuchapwa mabao 5-1 na watani wa jadi, Yamga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara juzi Uwanja wa BenjamÃn Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda dakika ya tatu na viungo, Mkongo Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 64 na 77, Mburkinabe Stephane Aziz Ki dakika ya 73 na Muivory Coast Pacome Zouazoua dakika ya 87 kwa penalti.
Refa Ahmad Arajiga wa Manyara alitoa adhabu ya penalti baada ya beki Mkongo, Henock Inonga Baka ‘Varane’ kumchezea rafu Nzengeli kwenye boksi na bao pekee la Simba limefungwa na Kibu Dennis Prosper dakika ya tisa.
Kwa ushindi huo, Yanga SC imefikisha pointi 21 katika mchezo wa nane na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi pointi mbili Azam FC ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.
Kwa upande wao, Simba SC baada ya kipigo hicho cha kihistoria, inabaki na pointi zake 18 za mechi saba nafasi ya tatu.