NIGERIA imefanikiwa kwenda Hatua ya Mtoano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Guinea-Bissau katika mchezo wa Kundi A usiku wa jana Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny Jijini Abidjan, Ivory Coast.
Bao pekee la Súper Eagle alijifunga beki wa ya Ligue2 Ufaransa, Opa Sanganté dakika ya 36.
Mechi nyingine ya Kundi A wenyeji Ivory Coast walitupwa nje baada ya kutandikwa mabao 4-0 na Equatorial Guinea Uwanja wa Olympique Alassane Ouattara Jijini Abidja.
Mabao ya Equatorial Guinea yalifungwa na nyota wanaocheza timu za madaraja ya chini Hispania, mshambuliaji Emilio Nsue wa Intercity mawili dakika ya 42 na 75, viungo, Pablo Ganet wa Alcoyano dakika ya 73 na Jannick Buyla wa SD Logroñés dakika ya 88.
Kwa matokeo hayo, Equatorial Guinea inamaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake saba, ikiizidi wastani wa mabao tu Nigeria na zote zinasonga mbele, wakati Ivory Coast imemaliza nafasi ya tatu pointi tatu, huku Guinea-Bissau ambao hawana hata pointi moja wakishika mkia.
Mechi za mwisho za Kundi B zote zilimalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2, Msumbiji na Ghana na Cape Verde na Misri.
Kundi hilo Cape Verde amefuzu kama kinara pointi saba akifuatiwa na Misri pointi tatu ambayo nayo inasonga mbele, wakati Ghana iliyomaliza na pointi mbili na Msumbiji pointi moja zote zinaaga mashindano.