NIGERIA YAITUPA NJE CAMEROON BAADA YA KUICHAPA 2-0 ABIDJAN


WINGA wa Atalanta ya Italia, Ademola Lookman usiku wa kuamkia leo amefunga mabao yote kuiwezesha Nigeria kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Cameroon katika mchezo wa Hatua ya 16 Bora Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.
Lookman alifunga bao la kwanza dakika ya 36, akimalizia kazi nzuri ya Mwanasoka Bora wa Afrika ambaye anacheza naye Serie A,Victor Osimhen mshambuliaji wa Napoli na bao la pili akafunga dakika ya 90 kwa msaada wa beki wa Fulham ya England, Calvin Bassey.
Mapema dakika ya tisa, Lookman alimsetia vizuri beki wa West Bromwich Albion ya England, Oluwasemilogo 'Semi' Ajayi akafunga, lakini bao likakataliwa kwa msaada wa Msaada wa Marudio ya Picha za Video (VAR).
Katika mchezo uliotangulia jana wa Hatua ya 16 Bora AFCON, Angola iliwatupa nje jirani zao Namibia kwa kuwachapa 3-0, mshambuliaji wa Al-Wakrah ya Qatar, Jacinto Muondo 'Gelson' Dala akifunga mawili dakika ya 38 na 42, kabla ya mshambuliaji wa Al Ittihad ya Misri, Agostinho Cristóvão Paciência 'Mabululu' kufunga la tatu dakika ya 66 Uwanja wa Bouaké mjini Bouaké.
Timu zote zilimaliza pungufu kufuatia wachezaji wake kutolewa kwa kadi nyekundu, Angola wakimpoteza kipa wa Primiero de Agosto, Adilson Cipriano da Cruz 'Neblú' dakika ya 17 na Namibia wakimpoteza beki wa Cape Town Spurs ya Afrika Kusini, Lubeni Pombili Haukongo dakika ya 40.
Angola na Nigeria zitakutana katika mchezo wa kwanza kabisa wa Robo Fainali AFCON ya mwaka huu Ijumaa ya Februari 2, Saa 2:00 usiku Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny Jijini Abidjan.

 



Post a Comment (0)
Previous Post Next Post