SIMON MSUVA AJIUNGA NA AL- NAJMA YA SAUDI ARABIA


MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva amejiunga na klabu ya Al-Najma yenye maskani Mji wa Unaizah inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Saudi Arabia.
Msuva anajiunga na Al Najma kufuatia kuachana na JS Kabylie aliyojiunga nayo Agosti mwaka jana akitokea nyingine ya Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia, Al-Qadsiah aliyoichezea kuanzia mwaka 2022.
Awali Msuva aliibukia akademi ya Azam FC mwaka 2010, kabla ya kuhamia Moro United 2011 na baadaye vigogo wa soka nchini, Yanga ambako alicheza hadi mwaka 2017 alikwenda Morocco.
Klabu yake ya kwanza ilikuwa Difaâ El Jadida aliyocheza hadi mwaka 2020 alipohamia Wydad Athletic alikodumu hadi mwaka 2022 akahamia Saudí Arabia.
Anarejea Saudi Arabia baada ya kuichezea Tanzania katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ambayo imetolewa Raundi ya kwanza tu baada ya kushika mkia katika Kundi F ikiambulia pointi mbili sawa na Zambia, wakiziacha Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zikisonga mbele.
Lakini Msuva amejiwekea rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kufunga kwenye Fainali mbili za AFCON, mwaka huu nchini Ivory Coast akifunga bao moja dhidi ya Zambia katika sare ya 1-1 baada ya Mwaka 2019 nchini Misri kufunga moja pia Taifa Stars ikichapwa 3-2 na Kenya.
Anamfuatia nyota wa zamani wa Simba, Thuwein Ally Waziri kufunga mabao kwenye Fainali hizo, ambaye yeye akifunga mabao matatu mwaka 1980 Tanzania ikichapwa 3-1 na wenyeji, Nigeria, 2-1 na Misri na katika sare ya 1-1 na Ivory Coast.
Mtanzania mwingine aliyefunga bao kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ni nyota wa zamani wa Simba SC, Mbwana Ally Samatta bao moja dhidi ya Kenya katika kichapo cha 3-2 mwaka 2019 nchini Misri.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post