BONDIA Hassan Mwakinyo amefungiwa mwaka mmoja na kutozwa Faini ya Sh. Milioni 1 baada ya kushindwa kupanda ulingoni kwenye pambano lake la Septemba 29 dhidi ya Mnamibia, Julius Indongo ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imeona
sababu zilizotolewa na Mwakinyo kwa kukataa kupigana hazikuwa na mashiko.
Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Mwakinyo kuzua taharuki kwenye mapambano yake baada ya Septemba 3, mwaka jana kugoma kuendelea na pambano raundi ya nne akiwa anaongoza dhidi ya mwenyeji, Liam Smith ukumbi Echo Arena Jijini Liverpool.
Kwa sababu hiyo, Bodi ya Ngumi za Kulipwa Uingereza (BBBC) ikamfungia bondia huyo kupigana nchini humo licha ya utetezi kwamba alipoteza begi Uwanja wa Ndege ambalo lilikuwa lina vifaa vyake ikiwemo viatu.
Mwakinyo alisema wenyeji wake walimpa viatu ambavyo vilikuwa vinambana ndio maana raundi ya nne akashindwa kuendelea kustahmilili maumivu na kujiuzulu.
Na kuhusu pambano na Indongo, Mwakinyo alisema Promota alimhadaa na kuwashirikisha maadui zake kwenye pambano hilo.